Wenyeviti wanne wateuliwa na Rais

0
242

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Wenyeviti wanne wa  Bodi za Wakurugenzi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais , Ikulu imeeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Juma Muhimbi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Kabla ya uteuzi huo Muhimbi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Transparent Finacial and Tax Consulting Services Ltd ya Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Anne Makinda ambaye muda wake umemalizika.

Dkt. Edmund Mndolwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Posta Tanzania (TPB) , ambapo anaendelea na wadhifa huo baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza.

Rais Samia Suluhu Hassan pia amemteua Profesa John Kondoro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambapo naye anaendelea na wadhifa huo baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza.

Profesa Valerian Silayo ameteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC).

Profesa Silayo anatoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Uteuzi wa Wenyeviti hao umeanza leo 16 Juni, 2021.