Dkt. Mathuki wa EAC ajitambulisha kwa Rais

0
233

Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Peter Mathuki, ambaye anakutana na Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kupokea maelekezo ya kazi.

Katika mazungumzo hayo Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Dkt. Mathuki kwa kushika wadhifa huo na amemtaka kutekeleza majukumu yake kwa juhudi na maarifa ili Wananchi wa Jumuiya wanufaike na Jumuiya yao.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya EAC kuna fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zitasaidia kukuza uchumi na kuendeleza miundombinu na kuongeza mshikamano.

Maeneo mengine ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Katibu Mtendaji huyo wa EAC ayafanyie kazi ni kuimarisha sekta binafsi ambayo ndio inategemewa katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana na kukuza uchumi pamoja na kuhakikisha Wananchi wanashirikishwa katika masuala mbalimbali yanayofanywa ndani ya Jumuiya hiyo.

Pia, amemtaka Dkt. Mathuki kusimamia vizuri mpango wa kukuza viwanda ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuweka mgawanyo mzuri wa viwanda utakaoepusha kuwa na viwanda vya aina moja.

Kwa upande wake Dkt. Mathuki amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpokea na kumpa maelekezo ya maeneo ya kutilia mkazo katika utendaji wake, na amemuahidi kuchapa kazi ili kutekeleza maelekezo na matarajio ya Marais wa nchi Wanachama wa EAC.

Dkt. Mathuki amekiri kuwa juhudi kubwa zinahitaji kuimarisha sekta binafsi, kuwawezesha vijana, kutekeleza miradi ya ushirikiano ikiwemo ujenzi wa miundombinu inayounganisha nchi na nchi na kupigania lugha ya Kiswahili ili itambulike katika mikutano ya Kimataifa.