Majaliwa: Taasisi ya Elimu ya Watu wazima fanyeni tafiti

0
150

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kufanya tafiti za kufuta ujinga na kutoa mafunzo na stadi, ujizi na ufundi kwa vijana ili kukuza uchumi na kuendesha viwanda.

Waziri mkuu ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Kimataifa la Miaka 50 ya Elimu Watu Wazima Tanzania katika ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa elimu katika kuboresha upatikanaji wa elimu ya watu wazima ili kupata wasomi wengi zaidi watakaokuwa chachu ya maendeleo kwa Taifa.

“Elimu kwa watu wazima inahitajika na ni muhimu sana ushirikiano ukawepo baina ya taasisi zinazotoa elimu hapa nchini na Serikali,” ameeleza Majaliwa

Akizungumza na wadau wa elimu waliojitokeza katika kongamano hilo waziri mkuu amesema tafiti zinaonesha kuwa watoto wana afya nzuri kutokana na uelewa wa wazazi kuhusu lishe.

“Tafiti zetu zimedhihirisha kuwa wazazi wamepata uelewa wa masuala ya lishe na kuwafanya watoto kuwa na afya nzuri ilayosaidia watoto kupata uelewa wa masomo yao mashuleni.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua kongamano hilo la siku tatu katika ukumbi wa maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo kaulimbiu ni, Elimu ya Watu Wazima kwa Maendeleo Endelevu.