Kiongozi wa mapinduzi aapishwa kuwa Rais  

0
121

Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali Kanali Assimi Goïta,  ameapishwa hii leo kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Kanali Goïta ameahidi kufanya uchaguzi huru na haki, uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari mwaka 2022.

Habari kutoka katika mji mkuu wa Mali, Bamako zinaeleza kuwa hakukuwa na sherehe kubwa wala picha zozote zilizopigwa wakati wa tukio hilo la kuapishwa kwa Kanali Goïta.
Kanali Goïta aliingia madarakani wiki mbili zilizopita baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kulazimisha kukamatwa kwa aliyekuwa Rais, Bah Ndaw ambaye naye alikuwa ni wa mpito pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Moctar Ouane.

Mapinduzi hayo ya kijeshi yalishutumiwa na Viongozi wa nchi Wanachama wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ambao pia waliisimamisha Mali uanachama kufuatia mapinduzi hayo ya kijeshi ambayo yalikuwa ya pili ndani ya kipindi cha miezi 9.