Gharama za ujenzi wa zahanati zatiliwa shaka

0
336

Kiongozi wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu Luteni Josephine Mwambashi amekataa kufungua mradi wa zahanati ya Mrao Keryo iliyopo wilayani Rombo  mkoani Kilimanjaro,  na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kufanya uchunguzi wa zaidi ya shilingi milioni 100 ambazo hazionekani matumizi yake katika ujenzi wa zahanati hiyo.
 
Luteni Mwambashi amefikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi wa kupitia nyaraka za ujenzi wa mradi huo, na kubaini kiasi hicho cha shilingi milioni 100 kati ya shilingi milioni 204.8 zilizogharimu katika ujenzi huo kutoonekana matumizi yake.
 
Amesema hajaridhishwa na nyaraka zilizopo, kwani zinaonesha Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) imechangia shilingi milioni 163.7 huku ikionesha gharama za ujenzi ni shilingi milioni 111.814 hadi mradi kukamilika, zikitofautiana na gharama za ujenzi za halmashauri ambazo ni shilingi milioni 204.8.
 
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo Mary Robert amesema kuwa ujenzi huo ulianza Oktoba 16 mwaka 2013, ambapo kwa sasa Wananchi zaidi ya mia mbili wanapata huduma katika zahanati hiyo ya Mrao Keryo.