Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini wanatarajia kuzindua chaneli mpya ya utalii itakayojulikana kama Tanzania Safari.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt Ayub Rioba amesema kuwa chaneli hiyo itakayozinduliwa Disemba 15 mwaka huu ni fursa kwa Watanzania kuvifahamu vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, – Dkt Abdulla Mohammed Juma amesema kuwa chaneli hiyo ya Utalii ni muhimu katika kuleta mabadiliko katika sekta ya utalii nchini.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dkt Freddy Manongi amesema kuwa kuanzishwa kwa chaneli hiyo ya utalii itakayojulikana kama Tanzania Safari kunatoa fursa kwa Watanzania kujua mambo mengi yanayohusu utalii.
Profesa Dos Santos Silayo ni Mtendaji Mkuu Wakala wa Huduma za Misitu Nchini (TFS) ambaye amesema kuwa suala la Utalii linaenda pamoja na uhifadhi wa mazingira, hivyo kuanzishwa kwa chaneli ya Utalii kutasaidia kutoa elimu kuhusu mazingira.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo wa Chaneli mpya ya Utalii anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.