Aliyekuwa Mhandisi wa maji Kongwa matatani

0
181

Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumchukulia hatua aliyekua Mhandisi wa maji wa wilaya Kongwa mkoani Dodoma ambaye kwa sasa ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Waziri Aweso ameagiza kufukuzwa kazi kwa Meneja huyo kutokana na tuhuma za upotevu wa shilingi milioni 600 zilizokua zitumike katika utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Mkoka wilayani Kongwa wakati akiwa Mhandisi wa maji wilayani humo.

Amechukua uamuzi huo baada ya kukagua mradi huo na kubaini fedha zilizotolewa haziendani na thamani ya mradi ambao unaonesha mapungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja na maji kuwa na chumvi nyingi, ambayo Wananchi wanadai si salama kwao.

Waziri Aweso ametaka Wahandisi wote waliohusika na upotevu wa fedha katika mradi huo wa maji katika kijiji cha Mkoka wilayani Kongwa kuhakikisha zinarejeshwa.

Hata hivyo Waziri Aweso ameahidi ifikapo Jumatatu ijayo, Serikali itapeleka mitambo kwa ajili ya kuchimba kisima kipya cha maji baridi katika eneo hilo.

Awali wakielezea changamoto zao, Wakazi wa kata ya Mkoka wamesema maji wanayopata kwa sasa yana chumvi nyingi, hivyo hawawezi kuyatumia na kuomba kuchimbiwa kisima kingine.