Heroin yawapandisha kizimbani

0
194

Watu wawili wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu mkoani Dar es salaam, wakikabiliwa na shitaka la kukutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin Hydrochloride zenye uzito gramu 194.93.

Washtakiwa hao Batuli Bakari na Saidi Abdalla wamefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa shtaka lao na Wakili wa Serikali Yusuf Aboud, mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo Ritha Tarimo.

Wakili Aboud amedai kuwa, Batuli na mwenzake walitenda kosa hilo Mei 5 mwaka huu maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni mkoani Dar es salaam.

Hata hivyo baada ya washtakiwa hao kusomewa shitaka linalowakabili, hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2019.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 17 mwezi huu kwa ajili ya kutajwa, na washtakiwa wamepelekwa rumande.