Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, ametangaza kufutwa kwa shamba lenye ukubwa wa ekari 4,087 maarufu kama shamba la Valeska lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Meru mkoani Arusha.
Waziri Lukuvi ametangaza uamuzi huo wakati akizingumza na Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Meru, akiwa katika ziara yake yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika mkoa wa Arusha.
Uamuzi huo umetangazwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuombwa kufanya hivyo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi amesema halmashauri ya wilaya ya Meru itawajibika kulipa fidia katika maeneo yanayohitaji fidia ambapo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni shilingi milioni 394.10.
Waziri Lukuvi ameainisha matumizi ya shamba lililofutwa kuwa ni ekari 1,500 kugawiwa kwa vijiji vitatu vya Kwaugoro, Valeska na Maloloni, ekari 1,028 zitatumika kwa shughuli za kilimo na ekari 1,559 zitatumika kwa matumizi mbalimbali kama makazi na biashara.