Hospitali zapata magari ya kubeba wagonjwa

0
175

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekabidhi magari 20 ya kubeba wagonjwa, yenye thamani ya shilingi bilioni 2.24 ambayo yatapelekwa kwenye vituo vya afya 13, hospitali za halmashauri 5, ya wilaya moja na ya rufaa ya mkoa moja.

Akikabidhi magari hayo katika hafla iliyofanyika ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amezitaka halmashauri nchini kutenga fedha za matengenezo, ili kuhakikisha magari hayo yanadumu kwa muda mrefu.

 “Iko tabia katika baadhi ya halmashauri kutosimamia haya magari kwa maana ya kutotenga fedha za kuyafanyia service kila inapotakiwa, lazima gari lihudumiwe ili litumike kwa muda mrefu zaidi,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amewaomba Wabunge waliopokea magari hayo wakayasimamie, ili yatoe huduma inayotarajiwa kwa Wananchi.

Waziri Mkuu amesema mwaka 2020 alikabidhi magari 50 ya kubebea wagonjwa kati ya 70 yaliyokuwa yamepangwa kutolewa ili kuboresha huduma za afya nchini, na kwamba magari hayo 20 ni yale yalibaki kukamilisha idadi hiyo ya 70.

Ameushukuru Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria kwa kuwezesha ununuzi wa magari hayo mapya,  kupitia mradi wa kuimarisha mifumo ya afya iliyo thabithi na endelevu.