Mtandao wa wizi wa mafuta bandarini wagundulika

0
323

Jeshi la Polisi wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es salaam, limegundua uwepo wa mtandao mkubwa wa wizi wa mafuta unaofanywa kwa kutumia mitambo inayotumika kuchimba visima vya maji ambayo imeunganishwa kuelekea katika bandari ya Dar es salaam.

Akizungumza na Waandishi wa habari, mkuu wa wilaya ya Kigamboni, -Sarah Msafiri amesema mtandao huo wa wizi umegundulika kufuatia jeshi la polisi kukamata gari maalum la kubeba mchanga kutumika kubeba mafuta.

Amesema watuhumiwa wote wamekimbia baada ya kuwaona askari polisi kupitia kamera za usalama za CCTV, ambazo wamezifunga katika nyumba moja iliyopo kwenye mtaa wa Kisota.

Hata hivyo Jeshi la Polisi wilayani Kigamboni limeanza msako wa kuwatafuta watuhumiwa hao na pia linaendelea na uchunguzi katika nyumba hiyo ambayo ina karakana.

Nyumba hiyo imebainika kuwa na ulinzi mkali ukiwemo uzio wa umeme, kamera za CCTV, mbwa, pamoja na eneo la kubadilisha muonekane wa magari yanayotumika kubebea mafuta.