Serikali za Tanzania na Misri zimetiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Megawati Elfu Mbili na Mia Moja katika maporomoko ya mto Rufiji.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo Ikulu Jijini Dar es salaam, Rais John Magufuli ametoa wito kwa wadau wote wa mazingira nchini kuunga mkono mradi huo kwa kuwa ni muhimu katika utunzaji wa mazingira.
Amesisitiza kuwa moja ya mambo yaliyozingatiwa wakati wa uanzishwaji wa mradi huo ni kuhakikisha hakuna uharibifu wowote wa mazingira unaoweza kujitokeza na kwamba kama kuna taarifa zozote zilizosema kuwa mradi huo unasababisha uharibifu wa mazingira hazina ukweli wowote.
Rais Magufuli ameongeza kuwa mradi huo wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji utakapokamilika, utasaidia nchi kuwa na umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na hivyo kuchochea ukuaji wa viwanda nchini.
Amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Kampuni ya Arab Contractors kutoka nchini Misri kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa ambao ni miezi 36 na hata ikiwezekana kuufupisha muda huo.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, mara kwa mara amekua akizungumza kwa njia ya simu na Rais Abdel Fatah Al-Sisi wa Misri ambaye amemuhakikishia kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.
Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuiomba serikali ya Misri kujenga miradi mingine ya kuzalisha umeme katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwa bado Tanzania ina vyanzo vingi kwa ajili ya kuzalisha umeme na inahitaji umeme zaidi.
Timu ya mazungumzo ya uanzishwaji wa mradi huo kwa upande wa Tanzania inaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi Dkt Leonard Chamuriho ambapo Rais Magufuli ametangaza kuwaongezea muda wa kustaafu wajumbe wote wa timu hiyo waliokua wastaafu mwaka huu na hivyo watastaafu baada ya kukamilika kwa mradi huo.
Dola Bilioni 2.9 za Kimarekani ambazo ni zaidi ya Shilingi Trilioni Sita za Kitanzania zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Hafla ya utiaji saini mkataba huo wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji imehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Misri Dkt Mostafa Madbouly, Spika wa Bunge Job Ndugai na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma.
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini akiwemo Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Mtume na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Epatha na Sheikh Mohamed Rafik wamehudhuria hafla hiyo na kufanya sala.
