Upanuzi wa uwanja wa Nduli mbioni kukamilika

0
360

Kukamilika kwa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Nduli uliopo mkoani Iringa kutasaidia kuongezeka kwa shughuli za utalii na kiuchumi katika mikoa ya nyanda za juu Kusini ukiwemo mkoa wa Iringa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya upanuzi wa uwanja huo, unaotarajiwa kuongezeka na kuwa na ukubwa wa kilomita 2.1 na kuwezesha kutua kwa ndege kubwa.

Kasesela amesema kinachofanyika hivi sasa ni kuhakikisha Mkandarasi anakamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa, ili mwishoni mwa mwaka huu ndege kubwa zianze kutua kwenye uwanja huo wa ndege wa Nduli.

Amesema uwanja wa ndege wa nduli ni chanzo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa Wananchi wa mkoa wa Iringa, hivyo ni lazima upanuzi wake ukamilike haraka ili Wananchi hao waboreshe maisha yao kutokana na shughuli za Utalii na biashara.

“Nimeomba msimamizi wa huu mradi ambaye ni TANROADS mkoa wa Iringa kuangalia namna ya kuharakisha kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na malipo kwa Mkandarasi ili alipwe kwa wakati na kazi ikamilike haraka, lakini pia upatikanaji wa mahitaji kama kifusi,” amesisitiza Kasesela.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole amesema kuwa, Mkandarasi wa mradi huo anafanya kazi masaa yote na kwa sasa ameongeza mitambo pamoja na Wafanyakazi huku kasi yake ikiwa ni ya kuridhisha.

Naye Yuan Rui kutoka kampuni ya Sinohydro Corporation inayofanya kazi ya upanuzi wa uwanja huo wa ndege wa Nduli amesema kuwa, mradi huo utakamilika ndani ya muda uliopangwa.

Kwa sasa uwanja wa ndege wa Nduli una ukubwa wa kilomita 1.6, na eneo linaloongezwa ni kilomita 2.1, hatua itakayoufanya kuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa zaidi ya zile zinazotua hivi sasa.