Mkumbo ataka kutumika vifaa vya ndani katika ujenzi

0
297

Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo ametoa wito kwa taasisi na kampuni zinazosimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali na binafsi, kutumia vifaa vinavyozalishwa na viwanda vya ndani.

Profesa Mkumbo ametoa wito huo wilayani Mkuranga mkoani Pwani, alipotembelea kiwanda cha Lodhia Steel Industries Ltd na kile cha Lodhia Plastic Industries Ltd.

“Tunawashukuru wanaoendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hapa Tanzania ambao wanatumia vifaa vinavyozalishwa hapa ndani katika ujenzi wao, lakini tunatambua pia kuna taasisi ambazo bado zina kasumba ya kutumia vifaa vya nje huku wakiamini kwamba viwanda vyetu vinazalisha vifaa vyenye ubora ambao sio sahihi lakini ukweli ni kwamba vifaa hivyo vina ubora ule ule sawa na vifaa vinavyotoka nje maana tuna taasisi zinazokagua ubora kama TBS,” ameeleza Profesa Mkumbo.

Aidha, amezitaka taasisi za umma na binafsi zinazodaiwa na viwanda hivyo baada ya kupatiwa vifaa kulipa madeni yao, ili viwanda hivyo viendelee kufanya kazi kwa ufanisi.

“Kuna baadhi ya taasisi za umma na binafsi ambazo wameweza kuwauzia vifaa na hawajalipwa na sisi kama Wizara inayohusika na kuwezesha biashara hilo ni eneo la muhumu tunalopaswa kulifanyia kazi, tutashirikiana nao kuwakumbusha wenzetu wa taasisi hasa za Serikali ambao hawajalipa ili waweze kulipa na viwanda hivi viendelee kufanya kazi na visisimame,” ameeleza Profesa Mkumbo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Lodhia Group Sailesh Pandi ameipongeza Serikali kwa kuwatembelea na kujionea utendaji kazi wa kiwanda hicho , pamoja na kujionea changamoto wanazokabiliana nazo.