Dangote afika Ikulu

0
206

Rais Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara Alhaji Aliko Dangote, ambaye amewekeza katika kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa saruji mkoani Mtwara.

Baada ya mazungumzo hayo, Alhaji Dangote amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara nchini na amemuahidi kuwa kampuni yake ambayo imewekeza dola milioni 770 za Kimarekani hapa nchini, itaendelea kuwekeza katika maeneo mengine ikiwemo mpango wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea.

Amesema, kutokana na kubadilika na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini,  atawahimiza Wafanyabiashara na Wawekezaji wenzake kuwekeza Tanzania kwa kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao.

“Tutaendelea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa Wananchi wa Tanzania, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ili kuunga mkono anachokifanya, sisi tutazalisha ajira,” amesema Alhaji Dangote.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Alhaji Dangote kwa uwekezaji alioufanya hapa nchini, na amemhakikishia kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wake na wawekezaji wengine unalindwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe, Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Masauni ambao wamehudhuria mazungumzo hayo kufanyia kazi changamoto zote zinazokikabili kiwanda cha saruji cha Dangote ili kiendelee kuzalisha inavyotakiwa na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.