Waziri Bashungwa amjulia hali King Kikii

0
999

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amewahimiza Wasanii nchini kuhakikisha  wanamiliki bima za afya zitakazowasaidia wanapokua wagonjwa.

Waziri Bashungwa ametoa rai hiyo mkoani Dar es salaam alipomtembelea nyumbani kwake msanii mkongwe wa muziki wa dansi nchini Kikumbi Mwanza Mpango maarufu kama King Kikii, ambaye anaendelea kupatiwa matibabu ya maradhi yanayomsumbua.
 
“Wizara itaendelea kufuatilia kwa ukaribu matibabu yako na kwa sababu daktari wako tuna mawasiliano ya karibu tutakuwa tunajua hali yako inavyoendelea kila siku,” amesema Waziri Bashungwa.
 
 Kwa upande wake msanii King Kikii amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kumtembelea na kumjulia hali, na pia amemuomba amfikishie salamu zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kumpongeza kwa kazi  nzuri anayoifanya ya kuliongoza Taifa. 
 
Mzee King Kikii ametumia nafasi hiyo  kuwaasa Wanamuziki na Wasanii nchini kuwa na nidhamu katika kazi, ili waendelee kufanya sanaa kwa muda mrefu.