Kaizer Chiefs yaifuata Simba SC

0
457

Kikosi cha Kaizer Chiefs kimeondoka Johannesburg nchini Afrika Kusini kuja Dar es Salaam, Tanzania kwa ajili ya mchezo wa mzunguko wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC.

Kocha wa Kaizer, Gavin Hunt amesema kuwa kikosi chake kina ari kubwa na kwamba wataulinda ushindi wao wa magoli 4-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa Mei 15, 2021 katika dimba la FNB, Afrika Kusini.

Endapo klabu hiyo itaindoa Simba SC katika hatua ya robo fainali, itakuwa imeweka historia ya kufika nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.

Kwa Simba kuweza kusonga mbele itahitaji ushindi wa magoli matano au zaidi, idadi ya magoli ambayo Kaizer Chiefs haijawahi kufungwa kwenye mashindano hayo makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika. Idadi kubwa ya magoli ambayo wamewahi kufungwa ni 4-0 (mara mbili) dhidi ya Esperance na Wydad Cassablanca, kipigo ambacho Simba ikifanikiwa kukitoa, mchezo utakwenda hatua ya penati.

Licha ya kwamba Kaizer Chiefs wana faida ya magoli hayo, lakini wanatambua kwamba Simba SC imekuwa ni timu imara sana inapocheza nyumbani, ambapo imeshinda mechi nne kati ya tano ilizokuwa mwenyeji katika msimu wa 2020/21.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibunni, Afrisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema “ama zetu, ama zao,” akimaanisha kuwa watapigana kufa na kupona na kwamba “Kaizer Cheifs kwa Mkapa hawatoki.”

Mchezo huo wa kusisimua utapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni.