Tanzania yashauriwa kupokea chanjo ya UVIKO19

0
353

Kamati maalum iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19) imependekeza kuwa serikali kuruhusu matumizi ya chanjo za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo.

Mapendekezo hayo yametolewa baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais hafla iliyofanyika Ikulu jijino Dar es Salaam huku ikipendekeza matumizi ya chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwani uchambuzi uliofanywa na kamati hiyo umeaini kuwa chanjo hizo zina “ufanisi na usalama,” ameeleza Profesa Said Aboud, mwenyekiti wa kamati hiyo.

Kamati imependekeza kuwa utoaji chanjo kwa wananchi uwe wa hiari, lakini kipaumbele zaidi kiwe kwa watoa huduma za afya, watumishi waliopo katika sehemu za utalii, viongozi wa dini, wazee, watu wenye magonjwa sugu, maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wasafiri.

Kamati pia imeeleza kuwa mwamko wa kupambana na wimbi la kwanza la ugonjwa huo lilikuwa kubwa kuliko wimbi la pili, hivyo imeshauri serikali kuwekeza nguvu katika mapambano dhido ya wimbi la tatu.

Aidha, serikali imeshauriwa kuimarisha huduma za afya sambamba na kutoa takwimu sahihi za UVIKO19, kukamilishwa kwa mwongozo wa UVIKO19, kuhimiza matumizi ya tiba asili na tiba mbadala, Tanzania ishiriki kwenye maamuzi yaliyofikiwa na Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU) na WHO huku ikifanya tathmini ya janga hilo kwenye uchumi na kuwa na mikakati ya kukuza uchumi.