Rais Samia Suluhu Hassan leo amefanya uteuzi wa watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali.
Katika uteuzi huo, Balozi Joseph Edward Sokoine ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na anachukua nafasi ya Meja Jenerali Wilbert Ibuge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Nenelwa Mwihambi ameteuliwa kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya Stephen Kagaigai, ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Rais Samia Suluhu Hassan pia amemteua Dkt. Edwin Mhede kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuchukua nafasi ya Mhandisi Ronald Lwakatale ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Sylvester Mwakitalu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua nafasi iliyoachwa na Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, na Joseph Pande yeye ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP) kuchukua nafasi ya Edson Makallo ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Uteuzi mwingine ni wa Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Salum Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na anachukua nafasi ya Meja Jenerali John Mbungo ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amempandisha cheo ACP Hamduni kuwa Kamishna wa Polisi (CP).
Neema Mwakalyelye yeye ameteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo Mei 15 na wataapishwa tarehe 18 mwezi huu kuanzia saa 9:00 alasiri Ikulu jijini Dar es salaam.