NEC yavionya vyama vinavyoshiriki chaguzi ndogo

0
359
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mwananchi, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo sasa kwenye majimbo na kata zinazofanya uchaguzi huo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa (Mst) Semistocles Kaijage katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 16 Mei, 2021 katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na Uchaguzi wa Udiwani katika kata tano za Tanzania Bara,

Jaji Kaijage amesema Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili kuuufanya uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.

Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika majimbo na kata hizo kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua wabunge na madiwani wanaowataka.

Uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Muhambwe na Buhigwe mkoani Kigoma na uchaguzi wa udiwani katika kata tano za Tanzania Bara, utahusisha idadi ya wapiga kura watakaopiga kura 303,965 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika kupigia kura ni vituo 793.