Bomba la mafuta kuwanufaisha Watanzania

0
295

Mikataba ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania iliyosainiwa hii leo Ikulu jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na viongozi wa nchi zote mbili unategemewa kuwanufaisha Watanzania kwa namna mbalimbali.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kutia saini, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, mbali na mradi huo kuongeza pato la Taifa, pia utazalisha ajira za kutosha kwa Watanzania.

Ameeleza kuwa mradi huo wenye urefu wa kilomita za mraba 1,443, ambapo kilomita za mraba 1,147 zitapita ndani ya mikoa nane pamoja na wilaya 24 nchini utawanufaisha Wakazi wa maeneo hayo.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ametaja eneo lingine la Tanzania ambalo ni ziwa Eyasi kuwa linategemewa kuwa na mafuta.

Amesema mbali na nchi ya Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo nayo inategemea kupata mafuta na watatumia bomba hilo kusafirisha mafuta yake.

Hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania imeshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, mgeni wake Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku moja pamoja na viongozi mbalimbali kutoka Uganda na Tanzania.