Watatu washikiliwa kwa tuhuma za mauaji Moshi

0
446
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale akionesha nyundo inayodaiwa kutumika kutekeleza mauaji ya kijana Rogers Kesy, Mkazi wa Mnazi, Manispaa ya Moshi.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa watatu kwa madai ya kuhusika na tukio la mauaji la kijana wa bodaboda Rogers Kessy, mkazi wa Mnazi- Kiboroloni, Manispaa ya Moshi.

Akizungumzia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale amesema mmoja wa watuhumiwa, Sifael Sarun alimkodisha marehemu ampeleke nyumbani kwake lakini baada ya kufikishwa nyumbani alimuua kijana huyo kwa kumpiga na nyundo kichwani na kisha kumnyonga na waya shingoni.

Kamanda Kakwale akionesha waya uliotumika kumnyonga kijana Rogers Kessy shingoni na kusababisha kifo chake.

Kamanda Kakwale amesema mara baada ya mtuhumiwa huyo kutekeleza mauaji hayo waliuweka mwili wa kijana huyo kwenye mfuko wa sandarusi na kuutupa pembeni mwa barabara kuu ya Moshi/ Himo.

Amesema Sarun alishirikiana na wenzake wawili Emanuel Sarun na Elia Laizer ambao wote wako chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi na kuwa uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Jeshi la Polisi limefanikiwa pia kukamata pikipiki yenye namba MC 880 AYR ambayo ilitumika kubeba mwili wa marehemu na kwenda kuutupa barabarani.