Balozi Mulamula : Mahusiano ya Tanzania nje ya mipaka ni imara

0
552

Uingereza imesema Tanzania ni mbia muhimu na wa miaka mingi wa maendeleo katika Jumuiya ya Madola na kwamba itaendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya uwekezaji, biashara, diplomasia na utawala bora.

Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika James Duddridge ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula,  muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Waziri Duddridge ameongeza kuwa ziara yake ya siku mbili hapa nchini ina lengo la kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya Uingereza na Tanzania.

Amesema Uingereza imekusudia kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi, mapambano dhidi ya rushwa na maboresho katika sekta za afya na elimu.

Kwa upande wake Balozi Mulamula amesema ziara hiyo ya Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika ni kielelezo cha Tanzania kuheshimika na kukubalika katika Jumuiya ya Kimataifa.

Amesema kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita ni diplomasia ya uchumi, ambapo Uingereza ni moja kati ya nchi tatu kubwa zinazowekeza hapa nchini na hivyo kuwa ni miongoni mwa Mataifa muhimu kwa Tanzania.

Balozi Mulamula amesema mazungumzo yake na Waziri Duddridge yamejikita zaidi katika masuala ya uchumi, kukuza biashara pamoja na kuiendeleza miradi mikubwa iliyokuwa ikitekelezwa na Uingereza.

Amesema ujio wa Waziri huyo wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika hapa nchini unathibitisha kuwa mahusiano ya Tanzania nje ya mipaka yake ni imara,  licha ya taarifa potofu zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya nje zikitilia shaka juu ya diplomasia ya Tanzania nje ya mipaka.