Kenya imezuia kuingia nchini humo ndege zote kutoka nchi jirani ya Somalia, ikiwa imepita wiki moja tu baada ya mataifa hayo mawili kutangaza kuwa zimemaliza tofauti zao za kidiplomasia zilizodumu kwa miezi kadhaa.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Anga ya Kenya imeeleza kuwa ndege zitakazoruhusiwa kutua nchini humo kutoka Somalia ni zile zinazobeba wagonjwa wa dharura na zile za Umoja wa Mataifa zinazofanya kazi ya kutoa misaada ya kibinadamu.
Hakuna sababu zozote zilizotolewa kwa ndege za Somalia kuzuiwa kuingia nchini Kenya, lakini taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Anga nchini Kenya imeeleza kuwa ni maelekezo kutoka Serikalini.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya nayo imetoa tangazo hilo.
Mara kadhaa nchi za Kenya na Somalia zimewahi kuingia katika mzozo wa kidiplomasia, na kuna wakati Somalia iliishutumu Serikali ya Kenya kwa kuingilia mambo yake ya ndani, shutuma ambazo Kenya imezikanusha.