Tanzania yawahakikishia Mabalozi ushirikiano

0
286

 
Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Mabalozi watano  walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana nao katika kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na nchi zao,  hususani katika masuala ya uchumi na ustawi wa jamii.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam wakati akipokea hati za utambulisho kwa nyakati tofauti za Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta za kilimo, viwanda, utalii, ufugaji na uvuvi, hivyo amewaomba kuwaleta Wawekezaji kutoka katika nchi zao kuja kushirikiana na Tanzania katika kuzitumia fursa hizo kwa manufaa ya pande zote.

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Mabalozi hao kufikisha salamu zake za shukrani kwa Marais wa nchi wanazoziwakilisha na kuwahakikishia kuwa yupo tayari wakati wote kushirikiana nao.

Mabalozi hao wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupokea hati zao za utambulisho, na kwa utayari wake wa kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano na nchi zao, na pia wamemuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha matarajio yake hasa katika uhusiano wa kiuchumi.

Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni Lebbius Taneni Tobias ambaye ni Balozi wa Namibia hapa nchini, Mary O’Nell – Balozi wa Ireland nchini, Dkt. Mehmet Güllüoglu ambaye ni Balozi wa Uturuki hapa nchini, Marco Lombardi ambaye ni Balozi wa Italia hapa nchini na Ricardo Ambrosia Sampio Mtumbuida ambaye ni Balozi wa Msumbiji hapa nchini.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupokea hati za utambulisho za Mabalozi tangu aingie madarakani Machi 19 mwaka huu.