Serikali kujenga soko jipya Kasanga

0
238

Serikali inatafuta eneo kwa ajili ya kuweka mwalo na soko la muda la kuuzia samaki katika Kata ya Kasanga halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa,  kufuatia mwalo na lililokuwa soko la kata hiyo kujaa maji baada ya kina cha maji cha Ziwa Tanganyika kuongezeka.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah baada ya kutembelea eneo hilo na kujionea uharibifu mkubwa wa miundombinu ya soko na mwalo kufunikwa na maji.

Amesema katika kipindi cha muda mfupi ujao Serikali inatafuta eneo hilo huku ikitafakari mipango ya muda mrefu ya kujenga sehemu ambayo ni salama zaidi kwa ajili ya kuweka mwalo na soko la kuuzia samaki katika kata hiyo ya Kasanga.

“Hii safari nimetumwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki kuangalia hali ilivyo, kwa jinsi nilivyoiona hatuwezi kufanya chochote hapa nitamshauri wizara tutafute eneo lingine na tutenge fedha za kujenga mwalo mwingine tutafute eneo ambalo litafanyiwa tathmini, hata maji ya ziwa yakiongezeka kusitokee athari ya namna hii.” amesema Dkt. Tamatamah.

Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/2021 inayoishia mwezi Juni mwaka huu, wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitenga shilingi milioni 78 kwa ajili ya ukarabati mdogo kwenye soko la Kasanga, shilingi milioni 748 katika soko la Kirando lililopo halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa na shilingi milioni 187 katika soko la Muyobozi lililopo halmashauri ya wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, lakini ukarabati haukufanyika kutokana na kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kuongezeka.

Akizungumzia athari iliyojitokeza kutokana na uharibifu wa miundombinu ya lililokuwa soko la Kasanga, Dkt. Tamatamah amesema soko hilo ambalo lilianza kutumika mwezi Machi mwaka 2020 uwekezaji wake umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.3 ikiwa ni gharama ya miundombinu na vifaa mbalimbali vilivyowekwa na Serikali na wadau ukiwemo Umoja wa Ulaya na kwamba limetumiwa kwa miezi isiyozidi miwili pekee ndipo maji yakaanza kujaa na kushindwa kutumika.

“Pamoja na hayo mwalo ulikuwa na viwango vyote kwa maana ya maeneo ya kupokelea samaki, kuoshea samaki na kuwapima kabla ya kuuza, eneo la kuuzia samaki wabichi, eneo la kuzalisha barafu na vyumba vya kugandisha samaki, eneo la kukaushia samaki kwa moshi, pamoja na vichanja vya kuuzia samaki na dagaa.” amefafanua Dkt. Tamatamah.