Watu wawili akiwemo mfanyabiashara raia wa Russia, wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu mkoani Dar es salaam kwa kosa la kughushi nyaraka.
Washtakiwa hao Shaban Matinde mkazi wa Mombasa nchini Kenya na Ramil Galimov raia wa Russia, wamefikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Adolf Verandumi mbele ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama hiyo Agustina Mbando.
Wakili Lema amedai kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Juni 4 mwaka 2013 wakiwa katika jengo la Ushirika wilayani Ilala mkoani Dar es salaam, kwa kutengeneza nyaraka za uongo kwa jina la Kampuni ya madini ya Kikunde wakijaribu kuonesha kuwa nyaraka hiyo imesainiwa na Mshindo Muyaga kwa niaba ya wachimbaji wadogo wa Kampuni ya Buhelo.
Washtakiwa hao wamekana shitaka linalowakabili ambapo Hakimu Mbando ametoa masharti ya dhamana kwa kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya shilingi milioni tano huku raia wa kigeni akitakiwa kuwasilisha hati ya kusafiria na kibali cha kazi.
Washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana, na kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 22 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.