Nyayo ya ‘Yesu’ kivutio adimu cha utalii Ruvuma

0
197

Unyayo wa binadamu wa kale ambao wananchi wa Kijiji cha Litembo mkoani Ruvuma huamini kuwa ni unyayo wa Yesu, umekuwa miongoni mwa vivutio vya watalii kutoka maeneo mbalimbali.

Salvius Nyamajabeni ni Mwenyekiti Baraza la Mila na Utamaduni wa kabila la Wamatengo amesema “kuna alama ya nyayo ya binadamu yenye vidole ambayo imekanyagwa juu ya jiwe miaka mingi iliyopita, sisi wananchi wa Litembo tunaamini kuwa Yesu amekanyaga kwa sababu haifutiki miaka yote,’’ anasema Nyamajabeni.

Amesema kila mwaka waumini wa Kikristo hupanda juu kilele cha jiwe la Litembo ambako kuna nyayo na kwenda kuhiji na kwamba eneo hilo pia limewekwa msalaba.

Mwenyekiti huyo anasema kijiji cha Litembo kina vivutio vingi vya utalii ambavyo havijatangazwa na kufahamika ambapo amelitaja jiwe la Litembo kuwa lina utajiri wa utalii wa kishujaa na kihistoria kutokana na mababu na mabibi za Watanzania takribani 800 waliuawa na wakoloni wa Kijerumani Machi 4, 1902 kutokana na kukataa kutawaliwa.

Mwenyekiti Mstaafu wa Kijiji cha Litembo, Paulo Mwingira anasema serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na wazee wa mila wa kabila la wamatengo wamejipanga kuhakikisha kuwa vivutio vyote vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo katika eneo hilo vinalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.