Rais Samia Suluhu Hassan: Uhusiano kati ya Tanzania na Kenya si hiari

0
234

 
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Kenya si wa hiari, bali ni wa lazima.

Akihutubia mabunge mawili ya Kenya, Bunge la Seneti na Bunge la Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Wananchi wa mataifa hayo mawili wanategemeana kwa kila hali, hivyo hawawezi kukwepa kushirikiana.

Amefafanua kuwa, uhusiano wa Tanzania na Kenya uko katika mafungu matatu ambayo ni udugu, historia na jiografia.

Rais Samia Suluhu Hassan ameelezea kushangazwa na baadhi ya watu wanaodhani kuwa Kenya na Tanzania ni nchi shindani, huku wengine wakidhani kuwa Tanzania ama Kenya inaweza kuendelea peke yake bila ya kutegemea taifa lingine.

Amewaita wendawazimu baadhi ya Wanasiasa kutoka pande zote mbili ambao wamekuwa wakihamasisha mambo yasiyokuwa ya msingi hasa uhasama baina ya Tanzania na Kenya.