CCM yazindua kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Muhambwe

0
148

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kassim Majaliwa, amewaomba Wakazi wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma kumchagua Dkt. Florence Samizi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa ndiye atakayewaletea maendeleo.

Majaliwa ametoa ombi hilo katika jimbo la Muhambwe,  kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo hilo,  uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Kibondo Mjini.

 Amesema wakimchagua Dkt. Florence watarahisisha shughuli za maendeleo katika jimbo hilo zikiwemo zile za ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama ya afya na barabara.

“Uchaguzi hauhitaji ushabiki wala mbwembwe bali umakini mkubwa ili kumpata kiongozi atakayekuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia na kuwasemea mahali popote, naye si mwingine ni Dkt. Florence Samizi, Tumchague Dkt. Florence hakuna kitakachoharibika,” amesema Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetenga zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuboresha hospitali ya wilaya ya Kibondo,  ili kuhakikisha wakazi wa wilaya hiyo wanapata huduma bora za afya.

Amesema Serikali imetenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo, hivyo wamchague Dkt. Florence kwa kuwa ndiye atakayeweza kusimia miradi hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Augustino Vuma amewaomba wakazi wa jimbo la Muhambwe wamchague Dkt. Florence kwa sababu ni kiongozi mnyenyekevu, msikivu na ndiye atakayeweza kushirikiana nao katika kutatua changamato zinazowakabili.

Naye mgombea wa ubunge katika jimbo hilo kupitia CCM Dkt. Florence ametumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa jimbo la Muhambwe kumpigia kura nyingi za ndio ili awe mwakilishi wao atakayeshirikiana nao katika kuhakikisha jimbo hilo linapata maendeleo.