Meli ya MV Mbeya II imepata dhoruba ya kupigwa na mawimbi makali wakati ikiwa safarini katika ziwa Nyasa kutoka Songea mkoani Ruvuma kuelekea Kyela mkoani Mbeya.
Dhoruba hiyo ilipelekea meli hiyo iliyokuwa na watu 87, ambao kati yao 25 ni Wafanyakazi wa meli, kukwama kwenye mchanga karibu na bandari ya Matema kwa saa kadhaa.
Akizungumzia tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Kyela Claudia Kitta amesema kuwa meli hiyo ilikwama na kutitia kwenye mchanga kutokana na uwepo wa mawimbi makubwa katika ziwa hilo.
Amesema mamlaka husika zilifika eneo hilo na kuitoa meli hiyo kwenye mchanga na kwamba hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza.
Amesema kwa sasa huduma za usafiri za meli hiyo zimesitishwa, ili wataalam waweze kuifanyia uchunguzi.
Mbali na kubeba abiria, meli hiyo pia ilikuwa imebeba tani 12 za mizigo.