Waliokaidi agizo la NEMC kuchukuliwa hatua

0
177

Na,Emmanuel Samwel TBC

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuwachukulia hatua Watendaji wa kiwanda cha Saruji cha Fortune Limited kilichopo Vikindu wilayani Mkuranga mkoani Pwani kutokana na kukaidi agizo la Wataalam wa mazingira wa baraza hilo.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo baada ya kutembelea kiwanda hicho, ambacho awali kililalamikiwa na Wananchi kwa kuchafua hewa kutokana na kuwepo kwa vumbi la saruji.

Ameeleza kusikitishwa na hatua ya uongozi wa kiwanda hicho cha saruji cha Fortune Limited ya kushindwa kutekeleza agizo la NEMC la kuzuia vumbi kutoka kiwandani hapo na kusambaa kwenye makazi ya watu.

“Nimefika hapa kiwanda kimesitisha uzalishaji na viongozi wamekimbia, hii yote ni kwa sababu wanajua wamekiuka maelekezo yanayotolewa na Serikali juu ya uzalishaji wa bidhaa usiozingatia taratibu za usimamizi na uhifadhi wa mazingira uliowekwa na Serikali, hivyo lazima hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao,” amesema Waziri Jafo.

Katika Ziara hiyo Waziri Jafo pia ametembelea na kukagua Kiwanda cha Chuma cha Lodhia Limited, na kuelezea kuridhishwa na namna kiwanda hicho kinavyozalisha bidhaa za chuma kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

“Serikali iko tayari kuwaunga mkono Wawekezaji ambao wanazingatia utawala wa sheria katika uzalishaji wa bidhaa pasipo kuathiri afya za Wananchi na miundombinu,” ameeleza Waziri Jafo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Saleish Pandit ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa vibali vya kuagiza chuma chakavu kutoka nje ya nchi, ili kukidhi mtahitaji ya kiwanda hicho ambacho kwa sasa kinazalisha tani 200 za chuma kwa siku ambapo uwezo wake ni kuzalisha tani 300, huku kikitoa ajira zaidi ya 1, 000 kwa Wananchi.