Wanamichezo watakiwa kujituma na kuwa na nidhamu

0
294

 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka Wanamichezo wote nchini kujiamini wanapokuwa kwenye michezo yao, ili waweze kushinda na kuitangaza Tanzania.

Amesema Wanamichezo wanapaswa kutambua kuwa wao ni wawakilishi muhimu wa Taifa,  na kwamba Serikali imeanza kutenga fedha kusaidia Wanamichezo wanaoshiriki michezo mbalimbali ya kimataifa. 

Dkt. Abbasi alikuwa akizungumza mkoani Dar es salaam kwenye futari iliyoandaliwa na kampuni ya PeakTime Media kwa ajili ya mabondia, wadau wa ndondi na pia kwa ajili ya kumuenzi Yassin Abdallah Ustadh aliyekuwa  Rais wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa nchini aliyefariki dunia mwezi Septemba mwaka 2020.

Amesisitiza Wanamichezo kujituma na kuwa na nidhamu wakati wote ili waeze kufika mbali.

“Serikali kwa sasa haitoi tu bendera kwa wanamichezo, tunatoa pia fedha na vitu vingine kwa ajili ya Wanamichezo wetu ili waweze kutuwakilisha vyema kwenye michezo ya kimataifa,” amefafanua Dkt. Abbasi.

Amesema kwa sasa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imefanya mageuzi kwa kuacha kuwa tu msimamizi wa sera za sekta za michezo, bali pia kuwa promota wa michezo kama ya ngumi hapa  nchini.

Kwa upande wake muandaaji wa futari hiyo, Suleiman Semunyu ameishukuru Serikali kwa kusimamia sekta ya michezo  na kuwa karibu na Wadau wa michezo mbalimbali.