Rais Samia Suluhu Hassan: Nitaongeza mishahara mwakani

0
232

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa atapandisha mishahara ya watumishi wa umma mwaka 2022.

Rais ameyasema hayo wakati akihutubia umati wa wafanyakazi uliojitokeza katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi kitaifa.

Ametaja moja kati ya sababu za kutoongeza mishahara mwaka huu ni athari zilizotokana na ugonjwa wa COVID-19 na kuathiri uchumi wa nchi nyingi duniani, ambapo uchumi wa Tanzania ulishuka hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 6.9.

Aidha, Rais ameahidi kupandisha madaraja na vyeo watumishi 85,000 hadi 91, 000 watakaogharimu shilingi bilioni 449 za kitanzania. Kulipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya shilingi bilioni 60 yatalipwa.

Watumishi wapya takribani 40,000 wanatarajiwa kuajiriwa hususani kwenye sekta ya elimu na afya watakaogharimu bilioni 239.

“Niwahakikishie wafanyakazi wenzangu, mwakani siku kama ya leo, nitakuja na package nzuri ya kupandisha mishahara. Tutahakikisha tunapandisha mishahara ya watumishi ikiwemo kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa sekta ya umma na sekta binafsi,” A
amesisitiza Rais wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Rais amefanya mabadiliko kwenye bima za afya na marejesho ya Bodi ya Mkopo ya Elimu ya Juu. Umri wa mtegemezi kwenye bima umeongezwa kutoka miaka 18 hadi 21, huku akifuta asilimia 6 ya ada ya uhifadhi wa mikopo ya wadaiwa.