Waandishi wa habari sauti ya bara hilo

0
187

Vyombo vya habari vya Afrika vimetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuhabarisha umma kuhusu masuala mbalimbali yenye maslahi na bara hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurgenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha wakati akizungumza na Viongozi na Wanafunzi wa chuo cha kijeshi cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini Burundi, waliotembelea ofisi za TBC zilizopo Mikocheni mkoani Dar es salaam.

Dkt. Rioba amesema kama ilivyo kwa majeshi ya nchi yanavyowajibika kulinda maslahi ya nchi zao, ndivyo ilivyo kwa vyombo vya habari ambavyo vina wajibu wa kulinda maslahi ya nchi pasipo kutumiwa vibaya na mataifa yasiyozitakia mema nchi za Afrika

“Vyombo vya Habari vinawajibika kulinda rasilimali za nchi na utamaduni wake kwa Afrika, kama vyombo vya Magharibi vinavyofanya kwa mataifa yao” amesema Dkt. Rioba

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo cha kijeshi cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini Burundi Jenerali Cassien Ntachebera amesema kuwa Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa katika kutetea maslahi ya nchi zao.

Jenerali Ntachebera ameeleza kufurahishwa na namna ambavyo mataifa ya Tanzania na Burundi yamekuwa yakishirikiana.

Awali, Viongozi na Wanafunzi hao wa chuo cha kijeshi cha Ukamanda na Unadhimu cha nchini Burundi walitembelea vitengo mbalimbali vya TBC ili kujionea namna shughuli za utangazaji zinavyofanyika.