Serikali imeagiza korosho zote inazonunua kwa wakulima kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kuanza kubanguliwa nchini.
Agizo hilo la serikali limetolewa mkoani Mtwara na Waziri wa Kilimo, – Japhet Hasunga wakati akizungumza kwenye mkutano wa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho.
Waziri Hasunga amesema kuwa mkakati wa serikali ni kuwanufaisha wakulima nchini, hivyo maamuzi ya kununua korosho ni sehemu ya maamuzi mema kwa manufaa ya wakulima wote.
Amesema kuwa wakati serikali inaendelea kukamilisha uhakiki wa wakulima wa korosho pamoja na kuendelea na malipo ya wakulima, mpaka sasa tayari wakulima 77,380 wamekwishalipwa, hivyo hakuna korosho itakayoruhusiwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi bila utaratibu maalumu na badala yake korosho zote zitabanguliwa nchini.
Waziri huyo wa Kilimo amesisitiza kuwa korosho zitakazoruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi ni zile Tani 2,000 pekee zilizonunuliwa mnadani na kampuni mbili kwa utaratibu uliokuwa ukitumika awali.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema kuwa serikali imedhamiria kuimarisha uchumi wa viwanda, hivyo haitakubali kuhujumiwa inapoendelea kuboresha uwekezaji, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda.