DC Nkumba : Ongezeni kasi kusimamia miradi

0
155

Mkuu wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita, – Said Nkumba amewataka viongozi ngazi ya kata hadi kitongoji wilayani humo kuhakikisha wanaongeza kasi katika ufuatiliaji na usimamizi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ili iweze kukamilika katika muda uliopangwa.

Nkumba ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyopokea fedha katika kipindi cha kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu kwenye kata za Butinzya, Ushirombo, Bulangwa, Bukombe, Lyambamgongo na Iyogelo.

Wakati za ziara yake, Nkumba ameelezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi katika kituo cha afya cha Lyambamgongo na zahanati ya Kagwe na kumuagiza Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Bukombe kuhakikisha anajipanga kupeleka Watumishi, ili mradi utakapokamilika uanze kuwahudumia Wananchi.

“Kaimu Mganga Mkuu anza kujipanga sasa ili mradi utakapokamilika Wananchi waanze kupata huduma za afya katika eneo lao,” ameagiza Nkumba.

Kwa upande wake Afisa Kilimo na Umwagiliaji wa wilaya hiyo Joseph Machibya kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe, amewataka Wakuu wa shule na Walimu wakuu wilayani humo kuhakikisha wanatoa taarifa za maendeleo ya miradi kila siku katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.

” Ofisi ya Mkurugenzi ipo wazi, hakikisheni mnatoa taarifa za maendeleo ya miradi ili kama kuna changamoto tuweze kuzishughulikia kwa wakati “amesema Machibya.

Miradi ya maendeleo iliyotembelewa na kukaguliwa na Mkuu huyo wa wilaya ya Bukombe, Said Nkumba ni pamoja na ukamilishaji wa maabara ya Biolojia na kemia katika shule za sekondari za Butinzya, Businda, Bukombe na Busonge.

Mingine ni ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa katika shule za msingi za Ushirombo na Bukombe pamoja na ukamilishaji wa zahanati ya Kagwe na kituo cha afya cha Lyambamgongo.