Bei ya mafuta ya kupikia yaendelea kupaa

0
240

Wafanyabiashara wadogo wa mafuta ya kupikia mkoani Dar es salaam, wameiomba Serikali kushughulikia upandaji holela wa bei ya bidhaa hiyo.

Wamesema katika kipindi cha ndani ya miezi mitatu, kumekuwepo na ongezeko la bei la wastani wa shilingi elfu tatu kutoka shilingi elfu  82 mwezi Januari hadi shilingi elfu  85  mwezi huu kwa katoni ya ujazo wa lita tatu kwa mafuta aina ya Korie,  ikiwa ni bei ya jumla.

Wafanyabiashara hao wamedai kuwa, kwa ndoo ya mafuta yenye ujazo wa lita kumi bei imepanda hadi kufikia shilingi elfu 35 kutoka shilingi elfu 28.

Wakizungumza na TBC kwa nyakati tofauti, Wafanyabiashara hao wadogo wa mafuta ya kupikia mkoani Dar es salaam wamesema kuwa, wamelazimika kupandisha bei kutokana na manunuzi kuwa juu.

Kwa upande wa Wafanyabiashara ya chakula ambao ndio watumiaji wakubwa wa mafuta wamesema kuwa, hali imekuwa mbaya ambapo wamelazimika kupunguza kiwango cha chakula wanachopika ili waweze kupata faida.

Tarehe 22 mwezi huu akijibu swali bungeni jijini Dodoma Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema kuwa, katika bajeti ya wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 wametenga shilingi bilioni 10 ili kuuwezesha Wakala wa Mbegu za Kilimo  Nchini (ASA)  kusaidia upatikanaji wa mbegu bora za alizeti na kwa bei nafuu kwa wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini na hivyo kuondoa adha ya upatikanaji wa mafuta.

Mahitaji ya mafuta ya kupikia nchini ni zaidi ya tani laki tano, wakati uzalishaji ukiwa ni tani laki mbili.