Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuagiza Mkuu wa mkoa wa Mwanza, – John Mongella kuwaweka ndani hadi kesho, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji mjini Mwanza (MWAWASA), Meneja wa Mamlaka ya Maji Vijijini mkoa wa Mwanza (RUWASA), Meneja wa Maji Vijijini wilaya ya Sengerema, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji mjini Sengerema na Mkandarasi baada ya kubaini changamoto kadhaa katika utekelezaji wa mradi wa maji wa Busurwangiri uliopo wilayani Sengerema.
Mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo ambao ni tegemezi wilayani Sengerema umegharimu shilingi bilioni 1.8, lakini hautoi maji na kusababisha Wakazi wanaoutegemea kunywa maji ya kwenye mashimo yenye tope.
Akitoa agizo hilo, Waziri Aweso amesema atakutana na Watendaji hao hapo kesho kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, kwa ajili ya hatua zaidi.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo akiwa katika ziara yake mkoani Mwanza, ziara yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuzungumza na watendaji wa taasisi zilizo chini ya wizara ya Maji.