Kampuni 800 za China kuwekeza Tanzania

0
162

Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini, ambao pamoja na mambo wamezungumzia biashara na uwekezaji.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Viongozi hao wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China nchini wakiongozwa na Janson Huang, wamempa pole Rais Samia Samia Suluhu Hassan kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli na wamempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais.

Wamemhakikishia kuwa Wafanyabiashara wa China wapo tayari kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita katika kukuza uchumi na kuinua ustawi wa Watanzania kupitia uwekezaji mkubwa wanaokusudia kuufanya kupitia kampuni zaidi ya 800 za China zilizo tayari kuwekeza Tanzania.

Wametaja maeneo ambayo kampuni zao zipo tayari kuwekeza kuwa ni katika viwanda vya kutengeneza simu, dawa za binadamu, magari, kuanzisha maeneo maalum ya viwanda na kuwawezesha Watanzania kupata ujuzi kupitia mpango wa elimu utakaotoa fursa kwa Watanzania kusoma vyuo vya Tanzania na China katika masuala mbalimbali yakiwemo uhandisi na utalii kwa ufadhili wa Serikali ya China na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa China.

Akizungumza na Viongozi hao, Rais Samia Suluhu Hassan amewashukuru kwa salamu zao za pole na pongezi na amewahakikishia kuwa Serikali yake itashirikiana nao katika uwekezaji na itaboresha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji ili matokeo ya uwekezaji huo yanufaishe pande zote mbili.

Pia amewahakikishia kuwa Serikali itafanyia kazi changamoto mbalimbali zinazokwamisha uwekezaji ikiwemo upatikanaji wa vibali vya kazi, kodi, ucheleweshaji wa malipo, urasimu, kushughulikia changamoto zinazojitokeza kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona.