Waziri Ndaki awataka watumishi kujiepusha na rushwa

0
136

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewataka watumishi wa wizara ya Mifugo na Uvuvi kujiepusha na vitendo vya rushwa huku akionya kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na vitendo hivyo hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yake.
 
Waziri Ndaki ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya mifugo uliofanyika jijini Dodoma.
 
Akizungumza na Wajumbe wa baraza hilo, Waziri Ndaki amewataka Watumishi hao kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za Serikali, huku akisema si vuzuri kwa mtumishi wa umma kutajwatajwa kuhusika na matukio maovu.
 
” Niwaombe Watumishi wote mjiepushe na vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria za nchi na taratibu za kazi, haipendezi kuona mtumishi wa umma anatajwatajwa  kwenye kashfa za rushwa, hili siyo jambo jema hata kidogo, epukeni rushwa,” ameonya Waziri Ndaki.
 
Ameongeza kuwa Watumishi wa Umma ni muhimu wakaheshimiana na kuzingatia nidhamu ya kazi, kujiepusha na vitendo vya ubabe na kudharauliana, huku akisema kuwa kila mtu katika kazi ana umuhimu wake.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti Baraza hilo la Wafanyakazi la wizara ya Mifugo na Uvuvi sekta ya mifugo ambaye ni Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia uvuvi Profesa Elisante Ole Gabriel amesema kuwa watahakikisha wanatekeleza maagizo yote ya Waziri Ndaki.
 
Amesema kupitia baraza hilo wataendelea kuboresha bajeti ya sekta ya mifugo ili kuwawezesha Wafugaji waweze kufanya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa mazoea.