Jumuiya ya Sharjah yakaribishwa kuwekeza Zanzibar

0
2218

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein ameikaribisha Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah kuzichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar.

Dkt Shein ametoa kauli hiyo Ikulu mjini Zanzibar alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Al Rawabi, – Abdallah Sultan Owais akiwa pamoja na baadhi ya viongozi wa Jumuiya hiyo.

Wakati wa mazungumzo hayo, Dkt  Shein amemueleza Mwenyekiti huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), tayari imeweka mazingira mazuri ya kuwekeza huko Zanzibar na kusisitiza kuwa milango ya uwekezaji iko wazi.

 

Amesema kuwa Zanzibar ina fursa nyingi za kuwekeza katika sekta mbalimbali,  ikiwemo ile utalii, viwanda, ufugaji na nyinginezo ambazo Jumuiya hiyo  ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah ina uzoefu.

Mbali ya kuitaka Jumuiya hiyo kuwekeza Zanzibar, Rais Shein pia amesisitiza umuhimu wa  kuwepo kwa ushirikiano na Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Zanzibar na kusisitiza kuwa Zanzibar iko tayari kufanya kazi na Jumuiya hiyo.

Ametumia fursa hiyo kupongeza mafanikio yaliofikiwa Jumuiya hiyo ya Sharjah ambayo aliitembelea mwezi Januari mwaka huu wakati alipokuwa katika ziara yake kwenye nchi za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE).

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wenye Viwanda ya Sharjah, – Abdallah Sultan Owais ameeleza kuvutiwa na mazingira ya Zanzibar na amemuahidi Rais Shein kuwa Jumuiya hiyo itahakikisha inaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria baina ya pande hizo mbili.