TAMISEMI kutumia Trilioni 7.6 mwaka wa fedha 2021/2022

0
138

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022, ambapo jumla ya shilingi Trilioni 7.6 zimeombwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali.

Akiwasilisha makadirio hayo Bungeni jijini Dodoma, Waziri Ummy amesema kwa mwaka wa fedha ujao wamepanga kutumia kiasi hicho cha fedha kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi Trilioni 4.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni pamoja na mishahara ya watumishi wa wizara hiyo inayokadiriwa kufikia shilingi Trilioni 3.9, huku zaidi ya shilingi Bilioni mia 7 zikitengwa kwa ajili ya matumizi mengine.

Makadirio ya bajeti ya TAMISEMI pia yanahusisha shilingi Trilioni 2.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo kati ya fedha hizo shilingi Trilioni 1.6 zitatokana na fedha za ndani na shilingi Trilioni 1.2 ni fedha za nje.

Kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Waziri Ummy amesema wanafanya uchambuzi na watachukua hatua kwa watumishi na watu wote waliohusika katika matumizi mabaya ya fedha za umma.

Kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ya mwaka wa fedha wa 2019/2020, halmashauri 53 sawa na asilimia 29 ya halmashauri zote 184 hapa nchini zimepata hati zenye mashaka na halmashauri 8 sawa na asilimia 4 zimepata hati chafu.