Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeandaa mkutano maalum utakaoshirikisha Wadau mbalimbali wa mazingira, wakiwemo Wawekezaji na Washauri elekezi wa Mazingira, lengo likiwa ni kujadili ucheleweshwaji wa mchakato wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA).
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amewaambia Waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa, mkutano huo utafanyika tarehe 17 mwezi huu.
Amesema kufanyika kwa mkutano huo ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo, la kutaka Wadau hao wakutane ili kuona namna ya kutatua changamoto zilizopo katika mchakato wa kufanya tathmini ya athari za mazingira.
“Kama tunavyotambua kuwa mchakato wa kufanya tathmini ya athari kwa mazingira ni wa kisheria, miradi yote ya maendeleo ambayo haijajengwa inatakiwa kupitia mchakato huo ili upate cheti cha mazingira ambacho kinatolewa na Waziri mwenye dhamana ya mazingira,” amesema Dkt. Gwamaka
Kuhusu vifungashio vya plastiki visivyokidhi viwango, Dkt. Gwamaka amesema suala hilo kwa sasa limefikia mwisho na endapo mtu atakutwa anauza au kutumia vifungashio hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Hatutegemei kuona kifungashio kisichokua na kiwango, elimu imeshatolewa vya kutosha na tulifanya kikao na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) na wametuhakikishia kwamba viwanda vipo na vinatengeneza vifungashio vyenye kiwango kulingana na matumizi ya mtumiaji, hivyo ukikutwa na kifungashio ambacho hakijakidhi kiwango utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza Dkt.Gwamaka.