Raundi ya tano ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) itapigwa kati ya Aprili 28 hadi Mei 02, 2021 katika viwanja mbalimbali hapa nchini.
Matajiri wa Chamazi Azam FC watakuwa wenyeji wa Polisi Tanzania katika Uwanja wa Azam Complex huku maafande wa Rhino Rangers kutoka Tabora wakiwa wenyeji wa Arusha FC katika dimba la Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Mchezo mwingine wa Aprili 29, mwaka huu utapigwa katika dimba la Karume mkoani Mara ambapo wenyeji Biashara United watakuwa wenyeji wa maafande wa Ruvu Shooting.
Aprili 30, kutapigwa michezo miwili, ambapo kule Mwadui Complex wenyeji Mwadui FC watakuwa wenyeji wa wagosi wa kaya Coastal Union na mchezo wa pili utapigwa katika dimba la Nelson Mandela mkoani Rukwa ambapo maafande wa Tanzania Prisons watawaalika vinara wa ligi kuu soka Tanzania Yanga SC.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa Mei 1, kutapigwa michezo miwili pia, kule Dodoma wenyeji Dodoma Jiji watakuwa wenyeji wa KMC ya Dar es Salaam huku Mabingwa watetezi wa kombe hilo Simba SC wakiwa wenyeji wa wana Nkurukumbi Kagera Sugar katika dimba la Mkapa.
Mchezo wa nane na mwisho katika hatua ya nane bora ya Kombe la Shirikisho utapigwa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo wenyeji JKT Tanzania watakuwa wenyeji wa washindi wa pili wa kombe hilo Namungo FC.
Awali, mechi hizi zilipangwa kuchezwa kati ya Aprili 2 hadi 4, lakini ziliahirishwa kupisha kipindi cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli.