Rais Magufuli ateta na Mwang’onda

0
2246

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa Apson Mwang’onda Ikulu jijini Dar es salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, Mwang’onda amemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lake la kumuona na kuzungumza nae na amempongeza kwa uongozi mzuri unaochochea kasi ya maendeleo hususani katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Mwang’onda ameitaja baadhi ya miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa chini ya serikali ya Rais Magufuli kuwa ni ule wa uzalishaji wa umeme katika mto Rufiji na ujenzi wa madaraja na barabara ambazo licha ya kurahisisha usafiri zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam.

“Mabadiliko ni makubwa sana ambayo yametokea, kuna miradi mikubwa mingi inafanyika sasa hivi, kwa hiyo mabadiliko ni makubwa kusema kweli na yote hayo ni kwa manufaa ya nchi, kwa hiyo nachoweza kusema amefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi”, amesema Mkurugenzi Mkuu huyo Mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda.

Ametoa wito kwa Watanzania wote kushirikiana na serikali ili iweze kutekeleza mipango yake kwa ufanisi na kwa manufaa ya Taifa.