Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema mafunzo ya mara kwa mara kwa Waandishi wa habari ni muhimu katika kuwajenga ili wawe Wazalendo na Taifa lao.
Dkt. Rioba ametoa kauli hiyo wakati akitoa semina maalum kwa Maafisa Wanafunzi wa Chuo cha Kijeshi cha Kamaka kutoka nchini Uganda waliotembelea ofisi za TBC zilizopo Mikocheni mkoani Dar es salaam, kwa lengo la kujionea namna uandaaji na urushaji wa habari unavyofanyika.
“Lazima tuwe na Wanahabari wanaojua historia, utamaduni, kutazama mambo kwa mapana pamoja na kujua dunia inavyokwenda kwa kufanya uchunguzi wa kina juu ya mambo yanayofanywa na nchi za magharibi dhidi ya bara la Afrika,” amesema Dkt. Rioba.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Waandishi wa habari kupita katika vyuo vya kijeshi ili kupata mafunzo ya aina mbalimbali yenye maslahi kwa Taifa.
“Leo hii ukisoma kwenye mitandao ya kijamii utashindwa kujua Mtanzania ni nani kutokana na yale yanayoandikwa na baadhi ya watu, mengine ni vya kubeza vitu vya msingi vinavyofanyika katika Taifa,” amesema Dkt.Rioba
Kwa mujibu wa Dkt.Rioba, TBC kama chombo cha umma kimekuwa mstari wa mbele katika kuhabarisha umma habari za uhakika juu ya utamaduni wa kiafrika, lugha ya Kiswahili pamoja na rasilimali zinazopatikana Tanzania yakiwemo madini.
Amesema Bara la Afrika linastahili kuombwa msamaha na mataifa ya magharibi kutokana na vitendo visivyostahili vilivyofanywa na mataifa hayo dhidi ya rasimali zake.
“Kwa zaidi ya miaka mia tano matajfa ya magharibi yamenyonya bara letu la Afrika na kutumia vyombo vyao vya habari kutangaza bara letu vibaya lakini sisi tumewasamehe,” amefafanua Dkt. Rioba.
Akijibu swali la mmoja wa Maafisa hao Wanafunzi aliyetaka kufahamu iwapo TBC imeathiriwa na mitandao ya kijamii katika harakati zake za kuuhabarisha Umma, Dkt.Rioba amesema kuwa TBC imejidhatiti katika kuuhabarisha Umma kupitia mitandao yake ya kijamii na hivyo kuifanya kuwa moja ya vyombo vya habari vinavyofuatiliwa na watu wengi.
“Teknolojia kwa sasa imekua kwa kiasi kikubwa, hivyo kama chombo cha Umma tumepanua wigo wa kuhabarisha umma kupitia mitandao ya kijamii ambayo habari zake husambaa kwa haraka zaidi,” amesema Dkt.Rioba.
Kwa Upande wake mkuu wa Shule Msaidizi na Mkufunzi Mkuu wa chuo hicho Brigedia Jenerali Octavius Butuuro amesema kuwa wamejifunza mengi kupitia TBC, na kwamba mafunzo waliyoyapata yatakuwa msaada kwa wanafunzi hao ambao wanajifunza mambo mbalimbali yakiweo ya kiuongozi.