Serikali kuendelea kuvithamini vyombo vya habari

0
162

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari, na itaendelea kuvitumia kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma akitokea Zanzibar, alikoshiriki Dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, – Abeid Amani Karume.

Amesema mchango wa vyombo vya habari nchini ni mkubwa, na kwa kutambua mchango huo Serikali itaendelea kuvithamini na kushirikiana navyo.

Wazìri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe, huku akivitaka vifuate sheria katika utekelezaji wa majukumu yake.

Ameongeza kuwa vyombo vya habari vilitoa  mchango mkubwa wakati wote wa msiba, pamoja na siku 21 za maombolezo ya kifo cha Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati John Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali inavitegemea sana vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma mambo mbalimbali inayoyafanya, hivyo haina budi kushirikiana na vyombo hivyo.

Ametoa rai kwa waandishi wote wa habari nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.