Ijumaa Kuu na ulaji wa nyama

0
207

Ijumaa Kuu ni siku ambayo Wakristo walio wengi wanakumbuka mateso ya Bwana Yesu Kristo msalabani pale Kalvari huku baadhi ya madhehebu yakifanya maigizo mbalimbali kuhusu mateso ya Yesu katika kuadhimisha siku hii bila kusahau ishara ile ya kutokula nyama siku hiyo.

Kwa wale wanaofuata utaratibu huu wa Ijumaa Kuu inayoadhimishwa kila mwaka ambapo mwaka huu 2021 imeangukia April 2, hawaruhusiwi kula nyama ya kuku, ng’ombe, mbuzi, nguruwe, kondoo na wanyama na ndege wowote wanaochinjwa mbali na kuwa ni halali.

Waamini wanashauriwa kutumia samaki, dagaa, mayai, kunde, mboga za majani na matunda kwa siku hii huku wengine wakiamini ni kwa kila Ijumaa ya Kwaresma.

Hii ni ishara iliyopo kwenye baadhi ya madhehebu ya Kikristo ikiwemo ya Katoliki, Kilutheri na Anglikana.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano (TEC), Padre Chesco Msaga akizungumza na TBC amesema Ijumaa Kuu ni siku ya “kujikania vitu unavyovipenda” si nyama pekee, ili kukumbuka mateso ya Yesu msalabani.

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yametokana na mapokeo mbalimbali ikiwemo ile ya kuwa Yesu aliteswa na kumwaga damu yake siku ya Ijumaa Kuu hivyo si vyema kula vitu vinavyomwaga damu katika siku hii huku baadhi ya mapokeo yakieleza kuwa nyama ilionekana kama chakula cha anasa kipindi cha nyuma hivyo watu walipaswa kuacha anasa zote ikiwemo ulaji wa nyama.