TFF yamfungia Mwakalebela

0
202

Kamati ya maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imemfungia miaka mitano Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Fredrick Mwakalebela kutokujishughulisha na mpira wa miguu ndani na nje ya nchi kwa miaka mitano kwa makosa ya kimaadili.

Mwakalebela pia ametozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000) za kitanzania baada ya kutiwa hatiani kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa mashabiki, wananchama na wapenzi wa Yanga dhidi ya vyombo vinavyosimamia mpira wa miguu nchini.

Uamuzi huo wa kamati umetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 73(4) cha kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013.

Mwakalebela alilalamikiwa kuwa Februari 19 mwaka huu aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kudai kuwa TFF, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) na Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi zinaihujumu timu ya Yanga, madai ambayo alishindwa kuthibitisha mbele ya kamati.

Shitaka jingine ni kutoa taarifa za uongo kwa waandishi wa habari kwa kudai kuwa anao mkataba wa mchezaji Bernard Morrison na klabu ya Simba.